Kuanza kutumia Shereko

Ingia kwa namba yako ya simu, unda tukio lako la kwanza, ongeza wageni na utume mialiko binafsi ya WhatsApp ndani ya dakika chache.

Imesasishwa 15 Oktoba 2026Dakika 3 kusoma

Shereko inakusaidia kualika wageni, kupokea majibu ya RSVP na michango, na kuwapokea wageni mlangoni, yote mahali pamoja. Mwongozo huu unakutoa kwenye akaunti mpya hadi kutuma mialiko yako ya kwanza.

1. Ingia kwa namba yako ya simu

Huhitaji nenosiri. Shereko inakuingiza kwa msimbo unaotumwa kwenye WhatsApp yako.

  1. Nenda shereko.com kisha bonyeza Anza bure leo (au Ingia).
  2. Weka Nambari ya simu kisha bonyeza Tuma nambari.
  3. Fungua WhatsApp, nakili msimbo wa tarakimu 6 na uuweke kwenye ukurasa wa Ingiza nambari, kisha bonyeza Thibitisha.
  4. Kama ni mara yako ya kwanza, andika Jina lako kisha bonyeza Endelea →. Unaweza pia kubonyeza Ruka kwa sasa na kuliweka baadaye kwenye Mipangilio.

Unaweza pia kuulizwa Ulisikia kuhusu Shereko wapi? Kama mtu wa Shereko alikusaidia kujisajili, andika jina lake ili apate sifa yake.

2. Jifunze mpangilio wa dashibodi

Ukishaingia unafika kwenye Dashibodi. Menyu ya kushoto (au mwambaa wa chini kwenye simu) ina:

  • Dashibodi: jumla ya matukio, wageni, kadi zilizotumwa na michango iliyokusanywa.
  • Matukio: kila tukio unaloandaa. Fungua moja kulisimamia.
  • Ujumbe: majibu ya wageni na RSVP.
  • Michango na Zawadi: fedha na orodha za zawadi za matukio yako yote.
  • Ripoti: muhtasari unaoweza kupakua.
  • Template: template zako za ujumbe wa WhatsApp.
  • Mipangilio: wasifu wako, muunganisho wa WhatsApp, salio na arifa.

3. Unda tukio lako

Bonyeza Tukio jipya kwenye dashibodi kisha fuata hatua nne: Aina ya tukio, Maelezo, Ujumbe na Kagua. Kisha bonyeza Unda Tukio. Soma Kuunda tukio kwa maelezo ya kila hatua.

4. Ongeza wageni na andaa kadi

  1. Kwenye ukurasa wa tukio, fungua kichupo cha Wageni kisha bonyeza Ongeza mgeni, au tumia Ingiza kubandika orodha nzima ya namba. Soma Kuongeza wageni.
  2. Fungua kichupo cha Kadi kuchagua muundo au kupakia picha yako. Jina la kila mgeni linajazwa lenyewe. Soma Kutengeneza kadi ya mwaliko.
  3. Bonyeza Jaribio kwenye kihariri cha kadi kutuma kadi ya majaribio kwenye WhatsApp yako na uikague.

5. Tuma mialiko yako

Bonyeza Tuma kadi (kwenye kihariri au ukurasa wa tukio). Shereko inakuonyesha watakaopokea kadi na jumla ya gharama kabla ya kutuma chochote. Thibitisha, na kila mgeni anapata kadi yake binafsi yenye vitufe vya RSVP: Atakuja au Hatakuja. Soma Kutuma mialiko.

Hatua zinazofuata

  • Washa michango ili wageni walipe kwa pesa za simu.
  • Andaa mapokezi ili wahudumu wa mlangoni waskani QR za wageni.
  • Pakua app ya Shereko usimamie kila kitu kwa simu.

Maswali ya mara kwa mara

Je, nahitaji nenosiri?

Hapana. Kila unapoingia unatumiwa msimbo wa mara moja kwenye WhatsApp yako, kwa hiyo hakikisha bado unatumia namba ya WhatsApp uliyosajili nayo.

Naweza kutumia Shereko bila tovuti?

Ndiyo. Bot ya WhatsApp ya Shereko inaweza kuunda tukio, kuandaa kadi, kuongeza wageni na kutuma mialiko ndani ya mazungumzo ya WhatsApp. App ya simu nayo inatumia akaunti ileile.

Kuunda tukio ni bure?

Ndiyo. Unalipa tu unapotuma ujumbe au kuwasha huduma za kulipia kama mapokezi. Bei huonyeshwa kila mara kabla ya kuthibitisha.

Nikikwama nimtafute nani?

Tutumie barua pepe hello@shereko.com au ujumbe WhatsApp. Kwa kawaida tunajibu ndani ya saa chache wakati wa mchana.

Bado unahitaji msaada?Timu yetu inajibu WhatsApp na barua pepe, kwa kawaida ndani ya saa chache mchana.

Tuandikie WhatsApp